Parliament of Tanzania

Mwongozo wa Spika kuhusu suala lililoombewa Mwongozo na Mhe. Devotha M. Minja (Mb)

MWONGOZO WA SPIKA KUHUSU SUALA LILILOOMBEWA MWONGOZO NA MHE. DEVOTHA M. MINJA (MB) KUHUSU KUTOJIBIWA KWA SWALI LA NYONGEZA LILILOULIZWA NA MHE. MARWA RYOBA CHACHA (MB) KWA

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO

MWONGOZO WA SPIKA

Waheshimiwa Wabunge, siku ya Jumatatu ya tarehe 02 Mei, 2016 katika kikao cha kumi cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Devotha M. Minja, (Mb), alisimama na kuomba Mwongozo wa Spika akitumia Kanuni ya 68(7) pamoja na Kanuni ya 46(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016.

Katika kujenga hoja ya mwongozo wake, Mhe. Devotha M. Minja (Mb) alinukuu baadhi ya maneno ya Kanuni ya 46(1) yanayosema kuwa "Waziri anayeulizwa swali atakuwa na wajibu wa kulijibu swali hilo kwa ukamilifu kama lilivyoulizwa." Alifafanua kuwa Wakati wa kipindi cha maswali na majibu, Mhe. Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti aliuliza swali la Msingi Namba 75 ambalo lilijibiwa na Mhe. Eng. Edwin Ngonyani (Mb), Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Baada ya majibu ya swali la msingi, Mhe. Marwa Ryoba Chacha (Mb) aliuliza maswali mawili ya nyongeza. Katika maswali hayo ya nyongeza, swali la pili ndilo lililalamikiwa na Mhe. Devotha M. Minja (Mb) kwamba halikujibiwa na Mheshimiwa Waziri. Hivyo ndio sababu ya kuomba Mwongozo huu wa Spika.

Kwa mujibu wa "Hansard," swali la pili la Mhe. Marwa Ryoba Chacha (Mb) aliliuliza kama ifuatavyo:-

"Mheshimiwa Naibu Spika, swali la pili, ninavyoongea sasa hivi hakuna mawasiliano kwenye hii barabara, imekatika! Daraja la mto Robana limekatika, Serikali iko tayari kuji-commit sasa hivi kupeleka hela zikajenge yale madaraja ambayo yamebomoka?"

Katika kutoa uamuzi wa kiti kuhusu Mwongozo wa Spika alioomba Mhe. Devotha M. Minja (Mb), nimejielekeza katika hoja au swali lifuatalo:-

Je, ni kweli kuwa swali la pili la nyongeza lililoulizwa na Mhe. Mwita Ryoba Chacha, (Mb) halikujibiwa?

Kanuni ya 46(1) iliyotumiwa na Mhe. Devotha M. Minja kuomba mwongozo huu inasema hivi:-

"Waziri anayeulizwa swali atakuwa na wajibu wa kulijibu swali hilo kikamilifu kama lilivyoulizwa, isipokuwa kwamba, kama jibu linalohusika ni refu au lina takwimu nyingi, Waziri atampa Mbunge muuliza swali nakala ya jibu mapema baada ya kikao kuanza, kabla ya muda wa kumjibu swali hilo haujafikiwa."

Kanuni hii aliyoitumia Mhe. Devotha M. Minja (Mb) inahusiana na maswali kujibiwa kikamilifu. Lakini pia Kanuni ya 45 fasili ndogo ya (3) inafafanua bayana kuwa:-

"Iwapo Spika ataridhika kuwa, swali la msingi au la nyongeza halijapata majibu ya kuridhisha, ataagiza lijibiwe kwa ufasaha zaidi katika kikao kingine cha Bunge."

Baada ya kupitia Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) nimeridhika kuwa swali la pili la nyongeza alilouliza Mhe. Mwita Ryoba Chacha (Mb) halikujibiwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano. Hivyo naupokea Mwongozo wa Spika alioomba Mhe. Devotha M. Minja (Mb) na naagiza kwa mujibu wa Kanuni ya 45(3) kwamba, Waziri husika aandae majibu ya swali hilo na atayatoa katika kikao chochote cha Mkutano huu wa Bunge unaoendelea.

Huo ndio mwongozo wangu.

Umetolewa leo Tarehe 24 Mei, 2016

Dkt. Tulia Ackson (Mb)

NAIBU SPIKA

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's