Parliament of Tanzania

Mwongozo wa Spika kuhusu suala lililoombewa mwongozo na Mhe. Ally Mohamed Keissy (Mb)

MWONGOZO WA SPIKA KUHUSU SUALA LILILOOMBEWA MWONGOZO NA MHE. ALLY MOHAMED KEISSY (MB) KUHUSU SWALI LA MSINGI ALILOULIZA

KWA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI

MWONGOZO WA SPIKA

Waheshimiwa Wabunge, siku ya Jumatatu ya tarehe 02 Mei, 2016 katika kikao cha Kumi cha Mkutano wa Tatu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Ally Mohamed Keissy, (Mb), baada ya kipindi cha maswali kuisha, alisimama kwa ajili ya kuomba Mwongozo wa Spika akitumia Kanuni ya 46(1) ya Kanuni za Kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016. Kanuni ya 46(1) aliyoombea Mwongozo Mhe. Ally Mohamed Keissy (Mb) inasema;

“Waziri aliyeulizwa swali atakuwa na wajibu wa kulijibu swali hilo kwa ukamilifu kama lilivyoulizwa, isipokuwa kwamba, kama jibu linalohusika ni refu au lina takwimu nyingi, Waziri atampa Mbunge muuliza swali nakala ya jibu mapema baada ya kikao kuanza, kabla ya muda wa kumjibu swali hilo haujafika.”

Katika kujenga Hoja ya mwongozo wake, alieleza kuwa ametumia Kanuni hiyo kwa kuwa swali lake alilouliza lilikuwa la msingi na vilevile alitaka swali hilo lijibiwe na ambaye alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Rukwa (Mhe. Eng. Stella Manyanya, (Mb) ambae kwa sasa ni Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa kuwa anajua mazingira ya Rukwa. Alimuona Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi kuwa hawezi kujua vizuri mazingira ya Mkoa wa Rukwa na Wilaya ya Nkasi. Aliendelea kusema kuwa lakini cha ajabu Mheshimiwa hakujibu swali hilo kwa ukamilifu.

Maswali ya kujiuliza kutokana na Mwongozo huu ni kama ifuatavyo:-

i. Je, Mhe. Mbunge anapouliza swali linalolenga Wizara fulani, anaruhusiwa kuchagua Waziri yeyote wa kujibu swali hilo?

ii. Je, ni kweli kuwa swali hilo la msingi alilouliza Mhe. Keissy halikujibiwa inavyotakiwa?

Kwa mujibu wa Kanuni ya Kanuni ya 39(1) inayoongelea maswali na taarifa ya maswali,

"Waziri anaweza kuulizwa maswali kuhusu masuala yoyote ya umma au jambo lingine lolote ambalo linasimamiwa na Ofisi yake,........"

Swali la Mhe. Ally Mohamed Keissy (Mb) Namba 81 kwenye Orodha ya Shughuli za siku ya tarehe 02 Mei, 2016 lililenga Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, hivyo Waziri anayehusika na Wizara hiyo alikuwa anawajibika kutoa majibu ya swali hilo la msingi la Mhe. Keissy (Mb).

Vilevile Ibara ya 63(3)(a) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 imeeleza kuwa;

"Kwa madhumuni ya utekelezaji wa madaraka yake Bunge laweza kumuuliza Waziri yeyote swali lolote kuhusu mambo ya Umma katika Jamhuri ya Muungano ambayo yako katika Wajibu wake"

Hivyo ni wazi kuwa Waziri anaweza kuulizwa swali lolote lile kuhusu mambo ya Umma lakini kwa sharti kwamba liwe katika Wajibu wake. Swali alilouliza Mhe. Ally Mohamed Keissy (Mb) ambalo alitaka lijibiwe na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi Mhe. Eng. Stella Manyanya, (Mb) halikuwa kwenye wajibu wake.

Aidha, Kanuni ya 39(13) inaeleza kuwa, swali aliloulizwa Waziri mmoja laweza kujibiwa na Waziri mwingine au Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kanuni hii imetoa fursa kwa Waziri yeyote au Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuweza kujibu swali lililoulizwa kwa Wizara nyingine. Kanuni hii imetoa uwanja mpana kwa ajili ya swali kujibiwa kiufasaha endapo Waziri mwingine yeyote au Mwanasheria Mkuu wa Serikali ataona anapaswa kufanya hivyo, lakini haijampa nafasi Mbunge mwenye swali kuchagua Waziri wa kumjibu swali lake.

Kanuni ya 46(3) ya Kanuni za kudumu za Bunge, Toleo la Januari, 2016 inasema kuwa;

"Waziri Mkuu au Waziri mwingine yeyote au Mwanasheria Mkuu wa Serikali anaweza kutoa majibu ya nyongeza kwa majibu yaliyotolewa na Waziri."

Vilevile madhumuni ya Kanuni hii, sio kwamba Mbunge muuliza swali anachagua Waziri wa kujibu swali lake la nyongeza bali ni uamuzi wa Waziri mwenyewe kama ataona kuna ulazima wa kuongeza majibu ya nyongeza kwa majibu yaliyotolewa na Waziri wa Wizara husika.

Kuhusu hoja kuwa swali la msingi la Mhe. Ally Mohamed Keissy, (Mb) halikujibiwa kikamilifu, nimefuatilia Taarifa Rasmi za Bunge (Hansard) na kuridhika kuwa swali hilo lilijibiwa kikamilifu na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Huo ndio Mwongozo wangu.

Umetolewa Leo Tarehe…………………………………………Mwezi Mei, 2016

Dkt. Tulia Ackson(Mb)

NAIBU SPIKA

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's