United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
MWONGOZO WA SPIKA ULIOOMBWA NA MHE. JOSEPH ROMAN SELASINI KUHUSU SUALA LA WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI KUTOJIBU SWALI LA MHE. DEVOTA MATHEW MINJA KWA UKAMILIFU
---------------
Waheshimiwa Wabunge, mchana wa leo tarehe 20 Mei, 2016 kabla ya kusitisha shughuli za Bunge Mhe. Joseph Roman Selasini (Mb) aliomba mwongozo wa Spika bila kutaja Kanuni husika kuhusu majibu ya swali Namba 205 ambalo lilielekezwa katika kujua ni kwa namna gani Serikali imejipanga kuboresha nyumba za Askari Magereza na Polisi kwani jibu liliotolewa linahusu uboreshashaji wa nyumba za polisi pekee.
Katika maelezo yake Mheshimiwa Selasini alieleza ifuatavyo naomba kunukuu:
“Askari Magereza wa nchi hii wanaishi katika hali duni sana na nitoe mfano tu katika Jimbo langu wanaishi katika vibanda vya mabanzi ambavyo kule tunajengea nyumba za nguruwe. Huu ni udhalilishaji mkubwa sana…Ni kwa nini usitolewe Mwongozo kwamba kwa ajili ya polisi uletwe mchanganuo na ionekane kwamba polisi watajengewa kiasi gani na Magereza kiasi gani tena kwenye maeneo yapi ambayo hawa Askari wa Magereza wanaishi kwa kudhalilika”
Waheshimiwa Wabunge, baada ya kuombwa Mwongozo huo Kiti kilielekeza kuwa majibu ya mwongozo huo yatatolewa baadaye.
Waheshimiwa Wabunge, kwa ajili ya ufafanuzi zaidi naomba kurejea swali Namba 205 lililoulizwa na Mhe. Devotha Mathew Minja(Mb) kama ifuatavyo:
“Askari wa Jeshi la Polisi na Magereza wanaoishi katika nyumba chakavu zisizokuwa na hadhi ikilinganishwa na kazi zao wanazofanya kwa jamii: Je, Serikali ina mpango gani kuwaboreshea askari makazi?”
Waheshimiwa Wabunge, baada ya kupitia Kumbukumbu za Taarifa Rasmi za Bunge ilibainika kuwa si kwamba swali la Mhe. Mbunge halikujibiwa kikamilifu na Mhe. Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ila Majibu ya Mhe. Waziri kuhusu swali husika hayakutoa mchanganuo wa nyumba ngapi zitajengwa kwa upande wa Askari wa Jeshi la Magereza.
Hivyo, kwa kuzingatia mwongozo ulioombwa na Mhe. Mbunge na uzito wa swali lililoulizwa, Kiti kimeamua kuelekeza swali hilo lirudiwe kuulizwa katika kikao cha tarehe 23 Mei, 2016 ili Serikali iweze kutoa majibu kwa ufasaha zaidi ikiwa ni pamoja na kutoa mchanganuo wa nyumba ngapi za Askari Magereza zitajengwa na katika maeneo gani.
Huo ndio Mwongozo wangu.
Umetolewa leo tarehe 20 Mei, 2016.
Mhe. Dkt. Tulia Ackson (Mb)
NAIBU SPIKA