Parliament of Tanzania

Mkutano wa Tisa wa Bunge waanza Mjini Dodoma

Mkutano wa Tisa wa Bunge la Kumi na Moja la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umeanza leo Jumanne tarehe 7 Novemba 2017 na unatarajiwa kumalizika tarehe 17 Novemba 2017 Mjini Dodoma.

Moja ya shughuli iliyofanyika katika Kikao cha Kwanza cha Mkutano huu wa Tisa ni Kiapo cha Uaminifu kwa Mhe. Janet Masaburi ambaye aliteuliwa na Mhe. Rais kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Aidha, mara baada ya kiapo hicho Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai alimtambulisha Katibu Mpya wa Bunge Ndg. Stephen Kagaigai na kuwaomba Wabunge wote kumpa ushirikiano katika utendaji kazi.

Kwa upande mwingine Mhe. Ndugai alimshukuru aliyekuwa Katibu wa Bunge Dkt. Thomas Kashililah kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi chake chote akiwa Mtumishi wa Bunge.

“Namshukuru sana kwa kazi kubwa aliyoifanya akiwa hapa Bungeni kwa takribani miaka thelathini na namtakia kila la kheri katika kazi yake Mpya,” alisema Spika Ndugai.

Mkutano huu wa Tisa wa Bunge unatarajiwa kujadili masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupitisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa mwaka wa Fedha 2018/2019. Kwa mujibu wa Kanuni ya 94 ya Kanuni za Bunge, Toleo la Januari, 2016 Bunge litakaa kama Kamati ya Mipango ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 63(3)(c) ya Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977 kwa kujadili na kuishauri Serikali kuhusu Mapendekezo ya Mpango wa Taifa.

Kwa upande wa Kipindi cha Maswali na Majibu, katika Mkutano huu wa Tisa, wastani wa maswali 125 ya Kawaida yanatarajiwa kuulizwa na Wabunge. Aidha, wastani wa Maswali 16 ya papo kwa papo kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu yanatarajiwa kuulizwa tarehe 9 Novemba na 16 Novemba, 2017.

Kuhusu Miswada ya Serikali katika Mkutano huu wa Tisa, Bunge pia linatarajia kupitisha Miswada Minne (4) ya Sheria ambayo itasomwa kwa hatua zake zote. Miswada hiyo ni:-

· Muswada wa Sheria ya Shirika la Mawasiliano Tanzania wa Mwaka 2017 (The Tanzania Telecommunications Corporation Bill, 2017);

· Muswada wa Sheria ya Wakala wa Meli Tanzania wa Mwaka 2017 (The National Shipping Agencies Bill, 2017);

· Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2017 [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No.4) Bill, 2017)]; na

· Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya wa Mwaka 2017.{The Drugs Control and Enforcement (Amendments), Bill, 2017}


Hon. Job Y. Ndugai

Speaker of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Mr. Stephen Kagaigai

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's