United Republic of Tanzania
Parliament of Tanzania
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Y. Ndugai (Mb) amefanya ziara katika Mamlaka ya Bandari Tanzania kwa lengo la kukutana na watendaji wa Mamlaka hiyo ili kupata maelezo ya kina kuhusu makontena yenye mchanga wa dhahabu yanayoshikiliwa na Mamlaka hiyo yaliyokuwa yasafirishwe kwenda nje ya Nchi.
Mhe. Spika ambaye aliambatana na Ujumbe wa Wabunge 10 kutoka Kamati Kamati mbili za Bunge za Nishati na Madini na ile ya Bajeti ambao pia waliongozwa na wenyeviti wao Mhe Dotto Biteko (Mb) kutoka Kamati ya Nishati na Madini na Mhe. Hawa Ghasia (Mb) Kutoka Kamati ya Bajeti amesema amelazimika kufanya ziara hiyo yeye mwenyewe kutokana na kuwepo na taarifa zinazochanganya hasa baada ya jana vyombo vya habari kuripoti kukamatwa kwa makotena mengine 256 tofauti na yale 20 yaliyoweza kupatikana wakati wa ziara ya Mhe. Rais wiki iliyopita.
“ Wananchi wengi wa Tanzania wana maswali mengi kuhusu biashara hii na kupitia kwetu kama wawakilishi wao watapa elimu ya kutosha kuhusiana na jambo hili ambalo hisia za watu zinaonyesha kwa sehemu kubwa tunahisi kama tunaibiwa” alisema Mhe. Spika
Kufuatia ziara hiyo, na baada ya kupatiwa maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari Ndg. Deusdetit Kakoko na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Ndg. Gilay Shamika, Mhe. Spika ameahidi Bunge kuunda Kamati Maalum kuchunguza biashara nzima inayohusiana na usafirishwaji wa mchanga wa dhahabu kwa kuitisha mikataba yote ya madini ili kujua nani wanafaidika na biashara hii ikiwa ni pamoja na kuangalia faida inayopatikana kwa watanzania na baadae kulishauri Bunge ni kitu gani kjifanyike na kwa wakati gani.
“Tungependa kujua ni nani anasimamia biashahara hii kuanzia kwenye source mpaka huko yanakokwenda madini yetu ili kujua maslahi yetu. Wakati umefika ambapo lazima tuchukue hatua tunapoona utajiri wetu unaondoka” alisisitiza Mhe. Spika
Awali, katika maelezo yake kwa Mhe. Spika, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini Ndg. Gilay Shamika alisema hivi sasa ni wastani wa Kontena elfu 50 hadi Elfu 60 za mchanga wa dhahabu ambazo husafirishwa kila mwaka na usafirishwaji huu umeanza tangu 1998 jambo lililomshitua Mhe. Spika na kusema kuwa kwa miaka yote hii inawezakana Tanzania imesafisha makontena milioni Moja jambo linalotia shaka katika biashara hii.