Parliament of Tanzania

Kamati yaishauri Serikali ifanyie marekebisho sheria ndogo zenye kasoro


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo imewashauri Mawaziri na vyombo vyote vilivyokasimiwa madaraka ya kutunga Sheria Ndogo ambazo Kamati imebaini kuwa na dosari wazifanye marekebisho yaliyopendekezwa haraka na kuyatangaza katika Gazeti la Serikali kabla ya Mkutano wa Saba wa Bunge.

Akiwasilisha taarifa ya mwaka ya utekelezaji wa majukumu ya Kamati kwa kipindi cha Januari 2016 hadi Januari, 2017, Mwenyekiti wa Kamati ya Sheria Ndogo Mhe. Andrew Chenge amesema mapendekezo ya kuzitaka mamlaka zinazohusika kuzifanyia marekebisho Sheria hizo yanatokana na Kamati kubaini kuwa majibu ambayo baadhi ya Mawaziri wamekuwa wakiwasilisha mbele ya Kamati, yamejaa ahadi za utekelezaji unaochukua muda mrefu wakati Sheria Ndogo zilizobainika kuwa na dosari bado zinaendelea kutumikana baadhi kuwa na madhara makubwa kwa wananchi kiuchumi na katika haki zao za msingi.

Aidha Mhe Chenge alisema kuwa katika utekelezaji wa majukumu Kamati yake ilibaini kuwa baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa zimekuwa zikinakili Sheria Ndogo kutoka katika Halmashauri nyingine neno kwa neno (copying and pasting) bila kufanya marekebisho ya msingi.

“Hali hiyo husababisha kunakili dosari za Sheria Ndogo hizo na wakati mwingine kutoendana na mazingira na mahitaji ya Mamlaka inayotunga Sheria Ndogo hiyo,” alisema Mhe Chenge.

Kutoka na hali hiyo Mhe Chenge alisema Kamati inazitaka Mamlaka za Serikali za Mitaa ziachane na mtindo wa kunakili Sheria Ndogo kutoka katika Mamlaka nyingine na zitunge Sheria Ndogo kulingana na mazingira halisi ya mamlaka husika.

Kwa upande mwignine Mhe Chenge alisema kuwa baadhi ya Sheria Ndogo zilizofanyiwa uchambuzi na Kamati zilibainika kuwa na makosa mengi ya kiuandishi na kiuchapaji, na baadhi kufanya rejea za vifungu katika majedwali kimakosa, zilikosewa kiasi cha makosa hayo yanasabisha tafsiri ya masharti ya Sheria Ndogo hizo kuleta mkanganyiko au kupoteza maana iliyokusudiwa.

“Baadhi ya dosari zilizobainika zimetokana na kukosekana kwa Wanasheria wa kutosha na wenye taaluma ya uandishi wa sheria katika Ofisi hizo”, alisema Mhe Chenge na kuongeza kuwa basi Kamati inashauri Serikali kufanya mapitio ya Sheria Ndogo zote zilizowasilishwa Bungeni tangu Mkutano wa Pili hadi sasa ambazo zimebainika kuwa na makosa ya kiuandishi na kiuchapaji ili kuondoa dosari hizo.

Pamoja na hilo Mhe Chenge alisema kuwa Kamati inaishauri Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuandaa program endelevu ya mafunzo kwa Wanasheria wa Wizara na Mamlaka za Serikali za Mitaa ili kuwajengea uwezo wa kuandika Sheria Ndogo ambazo zinakidhi matakwa na masharti ya Katiba, Sheria Mama na Sheria nyingine za nchi.

Mbali na hayo Mhe Chenge alisema pia Kamati imebaini kwamba wakati wa mchakato wa utungaji wa baadhi ya Sheria Ndogo haukushirikisha wadau kikamilifu, na kwamba kutoshirikisha wadau kunaleta changamoto ya utekelezaji wa Sheria Ndogo husika miongoni mwa makundi husika yanayoguswa na Sheria hizo.

“Hivyo basi Kamati inashauri mamlaka zote ambazo zimekasimiwa na Bunge mamlaka ya kutunga Sheria Ndogo kuzingatia kikamilifu ushirikishwaji wa wadau wanaolengwa na Sheria Ndogo yoyote,” alisisitiza Mhe Chenge.

Mhe Chenge pia alisema kuwa Kamati inashauri Ofisi ya Rais (TAMISEMI) ianze kutumia mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa upitishaji wa Sheria Ndogo katika hatua mbalimbali (The By – Laws Database).

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's