Parliament of Tanzania

Balozi wa China anayemaliza muda wake afika Ofisini kwa Spika Ndugai kumuaga

BALOZI wa China nchini LU Youqing amefika Ofisini kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Job Ndugai Jijini Dar es Salaam mapema leo kumuaga baada ya muda wake wa kukaa Tanzania kwisha.

Akizungumza na Spika Ndugai, Balozi huyo alisema kuwa muda wake wa kutumikia kama Balozi wa China hapa nchini umekwisha hivyo hana budi kuondoka ingawa angetamani kuendelea kubaki.

Balozi huyo aliongeza kuwa amefurahi kuona kuwa katika kipindi chake chote akiwa hapa nchini uhusiano baina ya Tanzania na China umezidi kukua.

“Ninafuraha kubwa wakati ninaporejea China kuona kuwa uhusiano wetu wa kihistoria umezidi kukua na kwamba kuna ongezeko kubwa la uwekezaji wa China hapa Tanzania na pia tumesaidia katika utekelezaji wa miradi mingi,” alieleza Balozi huyo.

Balozi huyo ambaye amesema kuwa Tanzania ni nchi yake ya mwisho kuhudumu kama Balozi aliongeza kuwa kwa sasa anarejea nchini China na akiwa huko ataendelea kujitikita katika shughuli za kudumisha uhusiano baina ya Tanzania na China.

“Tanzania ndiyo nchi yangu ya mwisho kuhudumu kama Balozi na nitakaporejea nyumbani (China) nitaendelea kufanya shughuli nyingine ambazo zinalenga kuimarisha uhusiano baina ya Tanzania na China,” alisema Balozi Youqing.

Kutokana na hilo Balozi Youqing alisema kuwa ingawa anarejea nchini China lakini yupo tayari kwa Tanzania kuendelea kumtumia kama Balozi wake katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali zitakozosaidia katika kudumisha ushirikiano baina wa nchi zote mbili.

“Nipo tayari kwa Tanzania kuendelea kunitumia kama Balozi wake aliyepo Nchini China, ninawakaribisha kwa mikono yote miwili tuendelee kufanya kazi kwa pamoja,” alisema Balozi huyo.

Kwa upande wake Spika Ndugai alimshukuru Balozi huyo kwa kazi kubwa ambayo ameifanya akiwa hapa nchini na kumueleza kuwa daima Watanzania wataendelea kumkumbuka kwa kazi nzuri aliyoifanya.

“Mimi binafsi katika kipindi chako ukiwa kama Balozi nimeshuhudia ongezeko kubwa la watanzania wengi tena wa hali ya chini wakisaifiri kwenda China kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kibiashara,” alisema Spika Ndugai na kuonegeza kuwa; kupitia fursa hiyo Watanzania wengi wameweza kujiajiri kupitia biashara ya kununua bidhaa toka China na kuja kuuza hapa nchini.

Mhe Spika pia alimshukuru Balozi Youqing kwa uchakapakazi wake katika kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo kupitia wataalamu kutoka nchini China.

“Unaondoka lakini utakapojisikia kurudi, sisi kama Bunge na Serikali kwa ujumla tupo tayari kukupokea kwa mikono miwili na kuendelea kufanya kazi na wewe,” alisema Spika Ndugai.

Mbali na hayo Spika Ndugai pia alimuomba Balozi Youqing kuendelea kuwa Balozi wa Tanzania atakaporejea nchini China kwa kuendelea kufanya shughuli ambazo zitasaidia katika kuimarisha ushirikiano baina ya pande zote mbili.

Hon. Dr. Tulia Ackson

Speaker

Legislative Role

Profile

Ask the Speaker / Comments

Ms. Nenelwa J. Mwihambi

Clerk of the National Assembly

Legislative Role

Profile

Ask the Clerk / Comments

View All MP's