|
|
| Home »Principal questions |
|
| |
 |
E-mail this to a friend |
 |
Printable version |
 |
Honourable Ernest Gakeya Mabina [CCM]
Geita Constituency |
|
| 9 |
103 |
REGIONAL ADMINISTRATION AND LOCAL GOVERNMENT |
Local Government |
8 November 2007 |
Kwa kuwa, Wilaya ya Geita kwa sasa inakadiriwa kuwa na jumla ya watu 810, 548 kati yao wanaume wakiwa 404, 735 na wanawake 405,813 ambao ni ongezeko la asilimia 3.4 na kwa kuwa idadi hiyo kubwa ya watu inahudumiwa na hospitali moja ya Wilaya, vituo vinane (8) vya Afya, Zahanati 44 na ina gari moja tu la kubeba wagonjwa ambalo ni bovu:-
(a) Je, Serikali inaona huo ni uwiano mzuri wa kutoa huduma za afya kwa wananchi wa Geita?
(b) Je, ni lini Serikali italeta magari ya kubeba wagonjwa kulingana na hali halisi ya Wilaya ya Geita?
|
| ANSWERS TO PRINCIPAL QUESTION #103 SESSION # 9 |
 |
Answer From Hon. Kombani, Celina Ompeshi
REGIONAL ADMINISTRATION AND LOCAL GOVERNMENT |
|
NAIBU WAZIRI, alijibu:-
Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ernest Mabina, Mbunge wa Geita, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-
(a) Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua hali halisi ya huduma za afya zinazotolewa kwa wananchi wa Wilaya ya Geita kuwa si za kuridhisha. Kulingana na idadi ya watu waliopo Wilayani Geita ambayo inakadiriwa kuwa ni watu 810,543 Wilaya inatakiwa kuwa na Hospitali tatu, vituo vya afya 16 na zahanati 81. Kwa sasa Wilaya ina Hospitali moja, vituo vya afya vinane na zahanati 51.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kuona upungufu huu imeanzisha mikakati ya makusudi ya kuboresha huduma za afya kwa wakazi wa Wilaya ya Geita. Miongoni mwa mikakati hiyo ni pamoja na kupandisha hadhi vituo vya Afya viwili kuwa Hospitali. Vituo hivyo ni pamoja na kituo cha Afya cha Karumwa katika Tarafa ya Msalala ambapo tayari huduma za upasuaji zimeanza kutolewa. Pia kituo cha afya cha Katoro katika tarafa ya Butundwe ambapo kiko kwenye mkakati wa kupandishwa hadhi kuwa hospitali.
Mheshimiwa Spika, Serikali pia kupitia mpango wa TASAF II imeanza kujenga zahanati 6 katika vijiji vya Lyulu, Kitongo, Ndelema, Buyagi, Msasa pamoja na Ibondo. Ujenzi wa zahanati hizi unatarajiwa kukamilika mwezi Disemba, 2007.
(b) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Geita inalo gari moja la kubebea wagonjwa ambalo lilikuwa bovu. Ubovu wa gari hilo ulitokana na ukosefu wa vipuri hapa nchini, vipuri hivyo vinapatikana nchini Korea Kusini, ambako gari hili lilitengenezwa.
Napenda kumfahamisha Mheshimiwa Mbunge kwamba vipuri vimeagizwa nchini Korea Kusini na vimekwisha patikana na gari hilo liko kwenye matengenezo Jijini Mwanza.
Mheshimiwa Spika, kama nilivyojibu swali Bungeni namba 185 la Mheshimiwa Msalika, Mbunge wa Nyanghwale, kwenye Mkutano wa nane wa Bunge lako Tukufu tarehe 9 Julai, 2007, nilieleza juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya Wilayani Geita, ni pamoja na suala la ununuzi wa magari mawili ya kubebea wagonjwa. Halmashauri ya Wilaya ya Geita katika Bajeti yake ya mwaka huu 2007/2008 imetenga fedha kwaajili ya kununua gari moja la wagonjwa litakalotumika katika kituo cha afya cha Karumwa.
Aidha kupitia maombi maalum yaliyowasilishwa Hazina, Halmashauri iliidhinisha Bajeti ya kununua gari lingine, hadi sasa hatua za manunuzi zimeshafanyika na magari yote mawili yameshalipwa fedha kiasi cha shilingi milioni 150 kwa kampuni ya Toyota Tanzania Ltd.
|
|
Records 1 to 1 of 23 |
|
|
|
|
|