|
|

Hon.Samuel Sitta(MP)
Online interactive forum with the SPEAKER |
|
" One of the core duties of the Legislature is to oversee the functions of the Government in power and advise it appropriately whenever any pertinent issue of national interest arises. " |
| 5th March 2009 - Dar es Salaam. |
|
|
 |
Procurement Plan for Goods, Works and Non-Consultancy Services in Financial Year 2010/2011
Read more |
|
Parliamentary Resources
National Website
Prime Minister's Office website
National Electoral Commission website
Africa4All project
|
|

|
|
|
|
| Who is the Prime Minister? |
When the results of a General Election are known the President appoints the Prime Minister who becomes the leader of the Government in the Parliament. The Leader of Government Business in the House is the Prime Minister who is assisted by all Ministers concerned primarily for organising the Business and for providing reasonable facilities for the House to debates matters about which it is concerned. The current Prime Minister is the Hon. Mizengo Kayanza Pinda MP. |
| Code of Conduct |
helps MPs understand their responsibilities to Parliament and the public. In addition to guidance, the Code also requires all Members to declare outside interest, like paid work or gifts |
Read more
|
|
|
|
|
| Home »Contribution |
|
| |
 |
E-mail this to a friend |
 |
Printable version |
 |
Mwandosya, Prof. Mark James[CCM]
Rungwe Mashariki Constituency |
|
|
|
|
|
| 8 |
16 |
4 July 2007 |
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2007/2008 Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano |
WAZIRI WA NCHI, OFISI YA MAKAMU WA RAIS, MAZINGIRA:
Mheshimiwa Naibu Spika, naanza kwa kuwashukuru wewe na Mheshimiwa Spika, kwa kutuongoza kwa kasi na viwango vya hali ya juu. Viwango vya michango ya Waheshimiwa Wabunge, nadhani utakubaliana na mimi hakika ni vya hali ya juu na ni michango ya kina sana. Nampongeza na kumshukuru vile vile mwenzangu Mheshimiwa Dr. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuwasilisha hotuba yetu kwa ufasaha mkubwa. Niseme kabla sijasahau kwamba, naunga mkono hoja yetu kwa asilimia 100.
Mheshimiwa Naibu Spika, nitachangia kwa kufanya majumuisho katika maeneo manne yafuatayo: Nitaanza kwa rambirambi na kutoa shukrani, nitapitia masuala ya kijumla na ya kisera kuhusu sekta ya mazingira, lakini vile vile nitapitia masuala ya utekelezaji wa sera, sheria na mikakati mbalimbali, baadaye nitafanya hitimisho.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa maana ya rambirambi, natoa rambirambi kwa familia, ndugu na marafiki kwa kifo cha aliyekuwa Mbunge mwenzetu, Marehemu Amina Chifupa Mpakanjia.
Mheshimiwa Naibu Spika, historia huandikwa kwa njia mbalimbali, mojawapo huwezi ukaamini lakini hivi vikaratasi ambavyo tunapeana ujumbe, nilikuwa napitia juu ya deski langu wiki hii nikijitayarisha na michango katika kuchangia hoja hii, nikakuta kikaratasi kimoja nilimwandikia Marehemu Amina Chifupa Mpakanjia 19 Aprili, 2007 kabla sijaondoka kwenda Dar es Salaam. Kwa bahati mbaya sikuweza kumpa lakini kilisema nakushukuru ahsante sana. Nimesahau ni kwa nini lakini hakupata huo ujumbe. Kwa sababu wote tunakwenda huko aliko, basi naamini nitapata siku moja ya kumshukuru.
Natoa rambirambi pia kwa wananchi wa Mwanza na Chama Kikuu cha Ushirika cha Nyanza, kwa kupotelewa na wenzetu wachapakazi wazalendo; aliyekuwa Mbunge mwenzetu hapa, Marehemu Stephen Kazi, Ndugu Hezron Ndoho na Ndugu William Kasubi. Vile vile natoa rambi rambi kwa waliofiwa na wale waliopotea katika ajali za barabarani huko Mbeya, Singida na Arusha. Kwa wote nasema Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahali pema peponi. Amen.
Mheshimiwa Naibu Spika, wananchi wa Rungwe Mashariki sijui niwashukuru kwa njia gani, wamekuwa na imani kubwa kwangu na wamekuwa ni mhimili mkubwa kwangu kisiasa. Tumekuwa pamoja katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi. Nawaomba tuendelee na umoja huo na mshikamano ili ndege ya maendeleo aliyozungumzia Mheshimiwa Edward Lowassa isituache. Vinginevyo tutabaki kwenye chumba cha abiria tukibishana nani atakaa kiti gani. Nadhani tunaelewana? Mimi naahidi kuendelea kuwatumikia kwa uwezo atakaonipa Mwenyezi Mungu, kwa bidii, juhudi, kwa nguvu zangu zote na kwa moyo wangu wote.
Namshukuru vile vile Mheshimiwa Makamu wa Rais, tumebahatika kufanya kazi chini yake. Msimamo wake, maelekezo yake na uongozi wake ni thabiti kabisa. Kwa siku hadi siku tunaongozwa na si mwingine bali ni Mheshimiwa Edward N. Lowassa, Waziri Mkuu, tunamshukuru kwa usimamizi wa Serikali.
Namalizia shukrani zangu kwa kuishukuru familia yangu, mke wangu Lucy, watoto wangu Max, Sekela, Emmanuel, wakwe zangu Johana na Digna na mjuu wangu Tusekile na watoto zaidi 100 ambao tunawalea kupitia Kituo cha Malezi cha Mama Lucy Mwandosya. Leo hii familia yote hii kubwa imewakilishwa kwenye gallery ya Spika na Mke wangu Lucy na vilevile mmoja wa watoto hao 100 anaitwa Cecilia.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa natoa majumuisho na majibu katika masuala ya kisera ya kijumla na vile vile ya kisheria. Ukizingatia Sheria ya Mazingira Namba 20 ya mwaka 2004, kuna mambo mawili yamezungumzwa na Waheshimiwa Wabunge na wameandika katika michango yao ya maandishi; nayo ni kuhusu usafi viwandani na uchafuzi unaotokana na mifuko ya plastic. La pili, wamezungumzia kuhusu elimu hasa elimu ya mazingira na kusisitiza umuhimu wake.
Mheshimiwa Naibu Spika, tutaendelea kutekeleza mpango wa elimu kwa umma kupitia radio, television, mikutano, mijadala, mikutano ya hadhara, mashindano ya usafi wa mazingira na kadhalika, lakini vilevile tutaendelea kutoa elimu mashuleni, vyuoni. Baraza la Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira lina wajibu mkubwa wa kusimamia na kusukuma elimu kwa umma kwa kushirikiana na Idara ya Mazingira katika Ofisi ya Makamu wa Rais. Vilevile kila sekta ina wajibu wa kusisitiza hili suala la elimu kwa umma katika suala zima la mazingira na asasi zisizo za Kiserikali zina wajibu mkubwa. Naomba kila mradi unaoanzishwa unaohusu mazingira, usisitize elimu kwa umma.
Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda kwenye masuala ya utekelezaji, nitaanzia na Maoni ya Kamati, ambayo yalitolewa kwa ufasaha mkubwa na Msemaji wa Kamati, Mheshimiwa Anastazia J. Wambura. Tumepokea na tutatekeleza maoni na ushauri mzuri wa Kamati ya Maliasili na Mazingira. Tumefaidika sana na michango yao wakati wote tunapokuwa nao na tunawashukuru sana kwa hilo.
Wamezungumzia vilevile kuhusu zoezi la kuwahamisha wafugaji kutoka Ihefu. Niseme tu kama Serikali, tumejifunza mengi, uzoefu tulioupata na ushauri utakaotokana na Tume Teule ya Mheshimiwa Rais, utatusaidia sana kama Serikali kuboresha utendaji hasa tunapokuwa na operation ya namna hiyo. Naomba Waheshimiwa Wabunge, tungojee tu matokeo hayo ya Tume ambayo imewasilisha ripoti yake kwa Mheshimiwa Rais. Pamoja na hayo niseme tu kwamba, hali ya mazingira ya Ihefu imebadilika, imekuwa nzuri. Changamoto kwetu ni kufanya mazingira hayo yaendelee kuwa bora.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu mifuko ya plastic, wachangiaji wote wameisifu hatua ya Serikali ya kupiga marufuku mifuko laini ya plastic, wote wamesema hatua za ziada zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku mifuko yote ya plastic. Wamekwenda mbali sana kuliko Serikali. Niseme tu tutazingatia hilo tutakapofanya tathmini ya utekelezaji wa agizo hilo, hatua za ziada zitachukuliwa ikibidi kwa mfano tunaweza tukaiga Rwanda ambao wamepiga marufuku kabisa hii mifuko ya plastic.
Lakini tumefanya nini NEMC? Katika kipindi hiki imekagua viwanda 18 lakini viwanda viwili ambavyo lazima nivitaje hapo Omar Packaging cha Mwalimu Nyerere Road na Saafa Plastic Limited cha Buguruni, vimebainika kuendelea kutengeneza mifuko. NEMC imewapa karipio, ni matarajio yangu kwamba watafuata hilo karipio vinginevyo NEMC ina uwezo wa kivifungia hivyo viwanda. Lakini vilevile tutaendelea kutoa elimu kuhusu suala zima la plastic na tutahakikisha kwamba, kwa zile plastic zinazoruhusiwa basi nembo zinawekwa ili tuweze kufuatilia zinatengenezwa na nani na ukaguzi utaendelea.
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu Kenya niseme wametuiga kwa sababu Waziri wa Fedha wa Kenya, Mheshimiwa Amosi Kimunya, katika Hotuba yake ya Bajeti ya 14 Juni, 2007, amepandisha ushuru wa plastic kwa asilimia 120 na amepiga marufuku mifuko laini ya plastic. Waziri wa Fedha, Mipango na Uchumi wa Uganda, Mheshimiwa Dr. Soluma naye katika hotuba yake ya bajeti ya Juni, 2007 amepiga marufuku mifuko ya plastic chini ya micron 30, mifuko wanayoiita wao Buvelo, ambayo sisi tunaiita Rambo.
Ameongeza ushuru kwa asilimia 120 kwa mifuko ambayo ni minene zaidi ya hapo. Mtakumbuka kwamba, hizi ni hatua ambazo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilizichukua mwaka 2006. Ninachotaka kusema hapa ni kwamba, hatua za pamoja Afrika Mashariki zitatusaidia sana kudhibiti mifuko hii.
Tathmini ya athari kwa mazingira imeweka bayana katika kifungu cha 81 mpaka 104, ulazima wa mradi wowote ule ambao umeainishwa kisheria kufanyiwa tathmini ya athari kwa mazingira na hakuna leseni yoyote itakayotolewa na mamlaka yoyote kutekeleza mradi wowote au miradi yoyote bila hati ya tathmini ya athari kwa mazingira. Katika miradi 25 ambayo mpaka sasa tumeifanyia tathmini ya athari kwa mazingira, miradi 24 imepewa hati na mradi mmoja tu ndio ambao umekataliwa.
Asilimia 40 ya miradi hiyo iko katika sekta ya madini, asilimia 20 katika sekta ya kitalii, asilimia 16 viwanda vya kemikali na vyakula, asilimia 12 ni nishati na asilimia 12 nyingine iliyobaki ni kwa ajili ya barabara, mafuta na ujenzi.
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie utekelezaji wa suala la tathmini ya haraka ya athari kwa mazingira ya ujenzi wa shule za sekondari ya Kwandede huko Karatu.
Hili ni eneo tete kimazingira, kuna chemichemi kama 29 na ziko katika lindi maji,ni chanzo mto Balai ambao unaelekea Ziwa Eyasi, ni bonde maarufu kwa kilimo cha vitunguu hasa kwa Kata za Balai na Mang¿oka.
Tarehe 10 mwezi wa Nne mwaka 2007, NEMC ilipokea barua kuhusu tatizo lililopo, ni kama mgogoro vile wa ujenzi wa Shule hiyo. Vile vile Mheshimiwa Slaa aliwasilisha maoni yake au malalamiko yake kwangu kuhusu suala hilo. Tarehe 4 mwezi wa Nne nilituma ujumbe wa wataalam kufanya tathmini kutoka Baraza la Usimamizi na Hifadhi ya Mazingira. Tumepokea rasimu ya ripoti, ripoti inakamilishwa, wadau wote hasa Halmashauri husika, Uongozi wa Mkoa pamoja na Mheshimiwa Mbunge watapata ripoti hiyo baada ya muda sio mrefu. Kuhusu utekelezaji wa Mkakati wa Kuhifadhi na Vyanzo vya Maji, natambua mchango wa Mheshimiwa Dr. Mzeru Nibuka na Mheshimiwa Lotto.
Mheshimiwa Naibu Spika, nimetembelea vijiji katika maeneo yao, baadhi ya vijiji hivyo katika milima ya Uluguru ni Kiloka, Kinole, Tawa, Matombo, Kibungo Juu, Msitu wa Kimboza, Ruvu, Maseyu na Mikese. Nimejifunza mengi sana hasa umuhimu wa elimu ya asilia au elimu ya jadi na utamaduni katika hifadhi ya mazingira.
Nilielezwa jinsi ya kupima wapi, au umbali gani, huwezi ukafanya shughuli za kilimo na makazi kwa kutumia mawingu yanapoonekana. Hii ni elimu ya jadi. Kwa maana hiyo, sio kweli kwamba walikuwa katika vilele vya milima. Nilielezwa kwamba mawingu sasa yameshuka kutokana na uharibifu wa mazingira; au yamepanda kutokana na uharibifu wa mazingira. Vinginevyo, zamani mawingu yalikuwa chini na ule ndiyo ulikuwa mstari ambapo mtu haruhusiwi kulima kupanda juu. Kwa hiyo, ilikuwa ni elimu kwangu.
Sasa miaka 50 kwa mfano mipaka iliwekwa Morogoro Mjini kutumia katani, kupiga marufuku kilimo na makazi katika eneo juu kidogo ya mji wa Morogoro. Milima ya Morogoro ya Uluguru ni tofauti sana na milima ya nyanda za juu Kusini. Maana niliombwa kwamba charity begins at home; ningeanzia kuwaondoa watu wa milima ya nyanda za juu Kusini.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba nyanda za juu Kusini milima yake ni uwanda wa juu unaotokana na kinachoitwa escapment kwa sababu ya bonde la ufa. Ni tofauti sana na milima ya Uluguru. Nawaalika Waheshimiwa Wabunge na wengine mje mwone jinsi hali asili inavyorudi baada ya kuwaondoa watu kwenye miteremko ya safu za milima ya Livingstone ili kulinda vyanzo vya maji. Hili halikufanyika na awamu hii ya nne, hapana. Lilifanyika wakati wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wakati kitu kilichokuwa kinaitwa Operesheni Sogea ili wote waliokuwa milimani washuke wapate huduma muhimu na hawajarudi mpaka leo. Imekuwa faida kubwa kwetu. Hii ni moja ya faida ya Operesheni Vijiji.
Sasa kwa upande wa Kiloka na Kinole wengi wameshuka, wengi walikuwa wakilima, lakini wanakuja kuishi chini na walikuwa na mguu mmoja juu, mguu mmoja chini. Kwa hiyo, hatujapata tatizo kubwa kuhusu hilo. Lakini tumeelezwa kuhusu kwa nini tunazingatia milima ya Uluguru.
Milima ya Uluguru ina umuhimu mkubwa sana kwa Taifa, kanda na kimataifa. Milima ya Uluguru ni moja ya maeneo 25 yenye umuhimu wa bionuwai ya misitu duniani na milima ya Uluguru inatambulika kimataifa. Milima ya Uluguru pamoja na milima mingine ya Tao la Mashariki ina aina 74 za wanyama wakubwa, yaani vertebrates na kati yao 13 hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani isipokuwa huko.
Lakini kuna mimea adimu na vile vile ni chanzo kikubwa cha maji Morogoro na Dar es Salaam. Sasa unaweza ukasema wabaki huko huko; lakini baada ya miaka 20 watakuwa wengi na madhara yatakuwa makubwa zaidi na maji yatapungua. Mimi naona afadhali hiyo operesheni iendelee. Ni ngumu, lakini tunafanya haya kwa kizazi cha sasa na kizazi kinachokuja. Ukilinganisha milima ya Uluguru na milima mingine ya Tao la Mashariki, sehemu ya milima ya Uluguru imeharibika zaidi katika kipindi cha miaka 20 iliyopita.
Mheshimiwa Naibu Spika, huwezi ukalinganisha na milima kama vile ya Ukaguru na Rubeho, huko ni kuzuri zaidi kuliko milima ya Uluguru. Nayo inatokana na stress kutokana na watu walivyozidi. Kwa hiyo, hamna utata tufanye nini. Nadhani wote tunakubaliana kwamba kwa kweli inabidi tudhibiti uharibifu uliopo na unaoweza kutokea kutokana na watu kuendelea kuishi katika vilele vya safu ya milima ya Uluguru.
Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba nimewasilikiza kwa makini sana wenzangu na ninawaelewa vizuri sana. Naomba wanielewe na watuelewe kwamba, kazi ya udhibiti wa mazingira ni ngumu. Kama unataka kupendwa, usiingie katika kazi hiyo. Sawa sawa na mambo ya dini, kama unataka kutenda dhambi usiende Kanisani, kwenye Msikiti au mahali kama hapo. Sababu ni moja! Unaposhughulikia kazi ya udhibiti wa mazingira, matokeo yake utayaona miaka 25, 30 kuanzia sasa. Kwa hiyo, ndiyo maana wanasema wameniambia wenzangu wanasema mazingira siyo dharura. Sikubaliani nao. Mazingira ni dharura.
Mheshimiwa Naibu Spika, nalinganisha sasa na wenzetu wa dini wanaofanya kazi huko, wao time frame yao ni kubwa zaidi maana yake wanazungumzia Ahera. Kwa hiyo, ndiyo maana nasema tunafanana fanana. Kwa hiyo, kama unazungumzia kupata kura 2010 mambo ya mazingira haya hayatakusaidia sana. Kwa hiyo, nimewaelewa ndugu zangu.
Utekelezaji wa mkataba wa usimamizi wa hifadhi endelevu wa hifadhi wa Ziwa Tanganyika. Burundi, Tanzania DRC Congo na Zambia, ndiyo tumetia saini mkataba huo. Masharti ya Mkataba karibu yote yamezingatiwa. Mamlaka ya Ziwa Tanganyika yameanzishwa mwezi wa Nne mwaka huu. Ilizinduliwa Dar es Salaam. Lakini sharti moja tu bado ni kwamba nchi zote ziwe zimeridhia mkataba kabla ya Wafadhili hawajatoa fedha za kutusaidia. Mpaka sasa Jamhuri ya Kimokrasia ya Congo haijaridhia. Kwa hiyo, tumekwama, lakini tunajitahidi, tuelewe wenzetu wametoka mbali sana.
Kwa hiyo, tuwavumilie, lakini hata hivyo katika wiki mzima hii, wiki mbili hizi nimekuwa na mazungumzo marefu na Mheshimiwa Balozi Halfani Mpango, Balozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DR - Kongo hapa nchini na vile vile nimekuwa na mazungumzo na Balozi Ngilangwa, Balozi wetu wa DRC Congo na wanalisukuma hili suala na wote kwa pamoja naamini tutafanikiwa hivi karibuni. Jana tu wamenitaarifu kwamba suala hili la kuridhia Mkataba lilikuwa limewekwa katika orodha ya shughuli za Bunge la Jamhuri ya Kimokrasia ya Congo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Balozi Ngilangwa alikuwa anafuatilia. Kwa hiyo, ni matumaini yetu kwamba wote tukiridhia, basi mkataba, mradi na mamlaka itakuwa imeanza rasmi kwa nchi zote husika.
Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu uharibifu wa misitu Mkoa wa Mbeya, Mheshimiwa Zambi amechangia na sana sana amezungumzia kuhusu Chumwa range kwa uchungu kabisa. Niseme tu Mheshimiwa Makamu wa Rais alipokuwa Mkoa wa Mbeya alipata taarifa kuhusu uharibufu huo kutoka kwa Mkuu wa Mkoa na alitoa maelekezo ambayo tutayafanyia kazi kwa pamoja na Mkoa, Wizara ya Maliasili na Utalii na Ofisi ya Makamu wa Rais. Nadhani pale ambapo mambo yameuzidi Mkoa, basi tutashirikiana katika hifadhi ya Chumwa Range. Lakini katika mazungumzo, vile vile ameulizia kuhusu upandaji miti maeneo ya wazi ya kiwanja cha ndege cha Songwe.
Niseme tu kwamba, Mheshimiwa Maua Daftari amenithibitishia kwamba hii shughuli ya kupanda miti katika maeneo yaliyo wazi ili kuzuia vumbi na kuleta mandhari nzuri katika kiwanja cha eneo wazi katika kiwanja cha ndege cha Songwe itaanza kufanyika katika kipindi cha mvua za masika kitakachoanza mwezi Novemba.
Lakini niseme tu vile vile kwa niaba ya Serikali, kwamba nawathibitishia wananchi wa Mkoa wa Mbeya kwamba fedha zipo za kumalizia kiwanja cha ndege cha Songwe na mchakato wa kumpata mzabuni karibu utakamilika. Niseme tu kwamba kiwanja hiki vile vile kipo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi.
Nawaeleza tu ndugu zangu wa Mbeya kwamba ni vyema Mkoa na kanda ujiandae na matumizi ya kiwanja hiki. Nilikutana na rafiki yangu mjini Arusha aliniambia: ¿Nimegundua dhahabu Mbeya.¿ Nikamwuliza, eneo gani? Akasema, siyo dhahabu, isipokuwa kiwanja cha ndege cha Songwe. Akasema sasa nanunua ardhi ili nihamie huko. Basi nawaeleza ndugu zangu wa Mbeya jinsi wengine wanavyokichangamkia kiwanja hicho.
Uchafuzi kutokana na viwanda hasa KTM Karibu Textile Mills, niseme kwamba, kabla ya mwaka 2005 viwanda vingi hapa nchini vilijengwa bila kuzingatia umuhimu wa tathmini ya athari kwa mazingira. Lakini Sheria ya mwaka 2004 inaitaka NEMC ivifanyie ukaguzi viwanda hivyo.
Kwa hiyo, Karibu Textile Mills imetakiwa na imeandaa mpango wa usimamizi wa mazingira, yaani environmental management plan na imeandaliwa na Clean Production Center ya Tanzania, Kituo madhubuti kabisa cha kwetu.
Kamati ya kusimamia utekelezaji inahusisha NEMC, Wizara ya Maji na Manispaa ya Temeke, tutaisimamia hiyo Karibu Textile Mills kwa karibu sana. Vinginevyo, NEMC itachukua hatua za zuio au prohibitory order.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, niseme mambo ya msingi tu kuhusu mazingira. Kila mwananchi na mtu yeyote aishiye Tanzania ana haki ya kuishi katika mazingira mazuri, safi na salama. Vile vile kila mwananchi, vikundi na jamii kwa ujumla wana nafasi na haki ya kuhusika katika maamuzi au kuyapinga maamuzi ambayo yanakwenda kinyume na maslahi yao na maslahi ya Taifa katika suala zima la hifadhi na usimamizi wa mazingira. Kila mwananchi ana haki na wajibu wa kuhusika katika sera, mipango na mchakato mzima wa usimamizi na hifadhi ya mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile msingi mwingine ni pale ambapo uwezekano upo kwamba matumizi ya maliasili na uchafuzi wa mazingira unaweza ukaleta madhara ambayo inakuwa vigumu kuyarekebisha, hivyo kukosekana kwa uhakika wa taarifa za kisayansi. Haiwezi kuwa sababu ya kutochukuwa hatua za tahadhari za kulinda mazingira.
Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa, mazingira ni urithi wa pamoja wa kizazi cha sasa na vizazi vinavyokuja, au kwa maneno mengine, tumerithi mazingira kutoka kwa watoto wetu, wajukuu zetu na vizazi vijavyo.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.
|
|
Records 78 to 78 of 78 |
|
|
|
|
|