|
|
| Home »Contribution |
|
| |
 |
E-mail this to a friend |
 |
Printable version |
 |
Mabina, Ernest Gakeya[CCM]
Geita Constituency |
|
|
|
|
|
| 20 |
16 |
25 June 2010 |
Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2010/2011- Wizara ya Katiba na Sheria |
Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili niweze kuchangia kwenye Wizara ya Katiba na Sheria. Kwanza kabisa, nataka kutoa pongezi kwa Wizara hii, kwa kazi kubwa anayoifanya ikiongozwa na Waziri Mathias Chikawe, Mbunge wa Nachingwea pamoja na Wafanyakazi wote wa Wizara hii ya Katiba na Sheria.
Mheshimiwa Spika, nimelazimika kusimama hapa kwanza kabisa nianze kwa kutoa shukrani kwa Chama chetu cha Mapinduzi, kikiongozwa na Mheshimiwa Dr. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuona na kuipa kipaumbele Wilaya ya Geita na kuanzisha Mkoa mpya wa Geita. Nashukuru sana kwa sababu lilikuwa ni lengo letu na madhumuni ya wananchi wa Geita. Kwa niaba ya wananhi wa Geita, tunaishukuru sana Serikali ya CCM kuweza kukubali ombi letu la kutuletea Mkoa mpya wa Geita.
Mheshimiwa Spika, pili, nimshukuru Waziri Mkuu ambaye ameweza kusukuma na kuweza kuleta Mkoa huu wa Geita. Katika kumbukumbu za Hansard mwaka 2002 wakati akiwa Naibu Waziri wa TAMISEMI, nakumbuka niliuliza swali la kuanzisha Mkoa wa Geita alijibu kwa kukataa lakini akanipa maelekezo, tumeyafuata maelekezo yale na leo hii kwa ajili ya busara yake na kwa wananchi wa Geita wamemuombea mpaka amekuwa Waziri Mkuu lakini ametimiza ahadi yake ya kutupa Mkoa wa Geita, tunashukuru sana.
Mheshimiwa Spika, huo ni mwanzo tu lakini unaweza ukakuta kwamba kuna uanzilishi na hata katika wanyama utakuta kwamba kuna wanyama wanaowinda sana lakini unakuta wanakula kidogo wengine wanakuja kumalizia. Kama simba akiwinda anaweza akapata nyama lakini anayekuja kufaidi ni yule fisi ambaye anakula yale makombo. Sasa tunaomba tu kwa sababu sisi ndiyo waanzilishi na ukiangalia katika takwimu utaona kwamba kuna vitu ambavyo tuliweza kuviwekea umuhimu mkubwa.
Mheshimiwa Spika, ukiangalia takwimu za mwaka 2002, utakuta kwamba Geita kulikuwa na watu laki saba na thelathini na tisa elfu (739,000). Jimbo la Geita lina watu (302,000), Jimbo la Busanda lina watu (323,000) Jimbo la Nyang’wale lina watu (159,000). Ukiangalia kuna Wilaya ambazo zimeingizwa katika Mkoa huu. Jimbo la Chato lina watu laki mbili na tisini na nne (294,000). Jimbo la Bukombe lina watu laki nne na themanini na tatu, kwa hiyo utaona kwamba Jimbo au Wilaya ambayo ilikuwa na watu wengi ni Wilaya ya Geita. Itakuwa maajabu wengine wanasema kwamba Makao Makuu yataenda Chato, naomba hilo lifutike kwa sababu walioanzisha ni wengine. Najua kabisa Geita kama Mkoa wa Geita Makao Makuu yatakuwa Geita. Nimelazimika kuyasema haya kwa sababu kuna mtu mwingine anaweza akaingilia hapa ikawa ni tabu tupu.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo maneno mazuri ya kupata Mkoa Geita, tumepata Wilaya ya Nyang’hwale, tumepata Halmashauri ya Nyang’hwale, kwa kweli ni faraja kubwa kwa wana Geita na wajue kabisa kwamba kuna wawakilishi wanaosilisha mawazo yao ndani ya Bunge lako Tukufu.
Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kazi kubwa ya kutulea sisi wana Geita, umefanya kazi kubwa sana, katika maelekezo yote uliyotoa tumeyafuatilia, hadi sasa hivi tumepata Mkoa wa Geita, lakini siwasahau Wabunge wa Geita kwa ujumla, namheshimu sana Mheshimiwa Marehemu Faustine Kabuzi Rwilomba alikuwa anaupigania sana Mkoa wa Geita, angekuwepo hapa mngeona cheche zake lakini mahali alipo tumuombee Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi, niombe familia yake ichukue jukumu hili la kuweza angalau tumheshimu katika familia ile na kuweza kuwa nao karibu kama inavyohitajika. Nimheshimu Mheshimiwa Musalika ambaye amekuwa mpiganaji mkubwa kwa kupata Mkoa huu, Mheshimiwa Lolesia Bukwimba pamoja kwamba amekuja hivi karibuni lakini ameweza kufanya kazi kubwa sana.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema haya, ninaomba kusema kwamba Wizara ya Katiba na Sheria, pesa iliyotengwa ni kidogo sana, wana kazi nyingi mno ukilinganisha na kazi zilizopo, ni sawa sawa na Wizara ya Elimu, ni sawa na Wizara ya Afya au ni sawa sawa na Wizara ya Mambo ya Ndani. Huwezi ukatenga shilingi bilioni 117 kwa kazi kubwa kama hizi wanazozifanya. Ni Wizara ambayo inategemewa katika kila sehemu, ni Wizara ambayo inategemewa na Chama Tawala na Vyama vya Upinzani. Hawa ndiyo wanaweza kuweka haki katika sehemu hiyo. Lakini tumekuja kuona kwamba wanapewa pesa kidogo mno hata ukipiga mahesabu tu utakuta kwamba kila Mkoa utakuwa unapata bilioni nne, ukigawa kwa kumi na mbili utakuta wanapata milioni mia tatu, milioni mia tatu ukigawa kwa Wilaya zake ni pesa kidogo mno. Unaweza ukaona kwamba ni pesa nyingi ambazo wamepewa, lakini ukijaribu kuzichambua utakuta kwamba wamepata pesa kidogo mno. Kwa hiyo, naomba kwa sababu tunapitisha basi niombe kwa siku zijazo Wizara hii iangaliwe kwa macho yote.
Mheshimiwa Spika, ninasema haya kwa sababu kuna sehemu ambazo zimekuwa na matatizo makubwa, kuna watu wana kesi wamo mahabusu, watu ambao wapo mahabusu ni wengi zaidi kuliko waliohukumiwa kesi zao. Kwa hiyo, unakuta pesa waliyopewa ni ndogo sana. Mfano katika Mahakama ya Wilaya ya Geita wameshindwa kuwalipa Wakalimani ambao wanaweza kufasiri kutoka lugha ya Kisukuma na Kiswahili. Kwa hiyo, kesi nyingi zimebaki pale pale. Huwezi ukasema kwamba watu wote wameshajua Kiswahili au wamejua Kiingereza, hakuna! Zinahitajika pesa za Wakalimani.
Mheshimiwa Spika, kuna kesi moja ambayo nimeifuatilia kwa ukaribu zaidi, kuna vijana ambao wana kesi yao wako mahabusu tangu mwaka jana kesi yao imekosa Mkalimani tu. Kwa hiyo, wamejikuta wamekaa mahabusu muda wote. Tuanzishe utaratibu ambao utakuwa ni mzuri zaidi. Mtu atakapokuja kuhukumiwa na muda aliokaa Mahakamani basi siku alizokaa Mahakamani zihesabike kama alikuwa amefungwa, ili zipungue katika kifungo chake. Mtu anaweza kuwa mahabusu miaka miwili, mitatu kesi yake haijasomwa Mahakamani sasa utakuwa humtendei haki mtu huyu. Naomba Serikali iwaongezee pesa katika eneo hili ambalo ni zuri zaidi na linaweza likasaidia na hii ni sehemu ambayo inatoa haki kwa kila mtu.
Mheshimiwa Spika, utakumbuka kwamba katika maeneo ya kwetu tumeanzisha Jeshi letu la Sungusungu. Jeshi hili limekuwa na manyanyaso makubwa kwani halijui sheria. Lakini kitu ambacho kinahitajika kuwaelekeza ni sheria ipi ambayo inaweza ikawasaidia. Tupo katika dhana ya ulinzi shirikishi pamoja na Sungusungu, ambao wameweza kusaidia matukio mengi ya ujambazi ya wizi na mambo mengine mengi ambayo yanaweza yakaleta vurugu katika Serikali yetu, lakini Jeshi hili badala ya kutendewa haki kwa sababu ya kutokujua sheria unakuta limekuwa na manyanyaso. Wengi wamefungwa, kama ndugu zangu wengine pale Kasamwa, Katoro na Nzera na maeneo mengi ya Geita unakuta wamekuwa na matatizo. Leo hii tulikuwa na tatizo moja la Sungusungu walishika majambazi walipotoka kule, majambazi walikuja kuwasingizia kwamba wameharibu mali zao, wameshaanza kushikwa na Polisi, lakini yote haya ni kwa kutokujua sheria.
Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana.
|
|
Records 1 to 1 of 20 |
|
|
|
|
|